
Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid.
Kibano hicho kilianza mapema asubuhi lakini moto
zaidi uliwaka jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti
hiyo iliyotengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya
bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ambayo ilitengewa Sh753 bilioni.
Wabunge wanawake 10 na wanaume wawili walichangia ikiwamo kutoa
shilingi.
Kambi ya Upinzani ilianza kuibana Serikali ikisema
imeweka rehani wananchi wake kutokana na kitendo chake cha kuchangia
kiasi kidogo cha fedha za maendeleo za wizara hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya kambi, Waziri Kivuli wa
Afya, Dk Anthony Mbassa alisema Bajeti ya Sh622 bilioni na fedha za
maendeleo ni Sh305 bilioni ambazo kati ya hizo, Serikali itatoa Sh54
bilioni tu, wakati washirika wa maendeleo watatoa Sh251 bilioni.
“Hii inaonyesha wazi kuwa Serikali imeendelea
kuweka rehani wananchi wake kutokana na bajeti kuendelea kuwa tegemezi
kwa wahisani,” alisema.
Kibano cha wanawake
Licha ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu
wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu
Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi,
walishindwa kuwashawishi wabunge hao waliokuwa wakililia nyongeza ya
bajeti.
Hoja hiyo, iliibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), Cecilia Paresso baada ya kuondoa shilingi akiitaka Serikali
itoe majibu ya sababu za kutoa Sh387 bilioni pekee kati ya Sh753 bilioni
za bajeti ya mwaka 2013/14, jambo ambalo limekwamisha utendaji kazi wa
wizara hiyo, ikiwa ni pamoja ya kushindwa kutekeleza Azimio la Abuja
kuwa kila nchi itenge asilimia 15 ya bajeti kuu kwa ajili ya Wizara ya
Afya ili kunusuru vifo vya kina mama na watoto.
Baada ya kauli hiyo wabunge kadhaa walisimama na
kuunga mkono hoja hiyo licha ya Mwigulu kulieleza Bunge kuwa Serikali
imepanga kuongeza kiasi cha fedha kilichobaki kabla ya Juni 31, mwaka
huu.
Hoja hiyo ilifafanuliwa na Malima ambaye alisema
Serikali imetoa Sh12 bilioni na kwamba tayari fedha hizo zimeshaingizwa
katika akaunti ya Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipia deni la Bohari
Kuu ya Dawa (MSD), ambalo ni Sh89 bilioni na deni la matibabu nje ya
nchi ambalo ni Sh21 bilioni.
“Kwa nini Bunge lilipitisha Sh753 bilioni wakati
likijua wazi kuwa haziwezi kupatikana, Watanzania watapataje huduma za
afya?” alihoji Paresso.
Jaji Werema alijibu akisema Azimio la Abuja ni la
hiari na hata kama nchi husika ikishindwa kulitekeleza haitapata adhabu
yoyote, huku akisisitiza kuwa Serikali haikupata fedha za kufikia
malengo ya azimio hilo na kuahidi kuwa kiwango cha fedha kilichobaki
kitaongezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.
No comments:
Post a Comment