
Serikali ya Rais Museveni inategemea kipato chake zaidi kutoka mkusanyo wa kodi
Bajeti katika
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatarajiwa kutangazwa. Ni wakati
ambapo mizani ya matumizi na mapato ya serikali huanikwa hadharani.
Biashara katika Jumuiya imekuwa mhimili imara wa uchumi wa nchi ya Uganda kukua, licha ya msukosuko katika masoko ya dunia.
Nchini Kenya wananchi wanatarajia
kuwa bajeti itaweza kuwalinda kutokana na mfumuko wa bei pamoja na
kiwango kikubwa cha kodi inayotozwa.
Hali ni hiyo hiyo nchini Uganda kwa mujibu wa mwandishi wetu wa Kampala Ali Mutasa.
Kiokozi cha Uganda kiuchumi, kwa mujibu wa Rais
Yoweri Museveni - ni Kilimo, Viwanda, Huduma, na Tetama - yaani,
teknolojia ya taarifa na mawasiliano (ICT).
Katika sekta hizo zote
nne, mali huzalishwa na nafasi za kazi hubuniwa. Hivyo bajeti ya mwaka
2014/15 itamakanikia sekta hizo nne.
Mwaka huu wa fedha, ingawaje, wafadhili waliikatia misaada bajeti - karibu robo.

Uganda ilipitisha sheria kali zaidi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja
Si kwa sababu za kiuchumi, bali za kisheria; Uganda ilipoamua kupitisha sheria kali zaidi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Labda bajeti itaongelea kirefu athari ya kukatwa msaada huo.
'Faida ndogo, kipato kidogo'
Kipato cha serikali zaidi kinatokana na kodi.
Zaidi ya thuluthi mbili mwaka huu wa fedha serikali ikitegemea mkusanyo
wa kodi, zaidi ya trilioni 8.
Lakini kukazuka tobo la kama $milioni 148, sababu ya baadhi ya makampuni kushindwa kulipa kodi.
Mojawapo ya sababu ni vita vya Sudan Kusini ambavyo vilivuruga biashara na Uganda, iliokuwa karibu $1bn, kila mwezi.
Uchumi haukukua kwa karibu 7%, badala yake
ulizidi 5%, hii ikimaanisha faida za makampuni fulani zilikuwa chini
hivyo kipato cha serikali kupungua.

Shilingi ya Uganda imeshuka dhidi ya sarafu kama dola ya Marekani
Sekta binafsi ambayo inatiliwa shime na serikali
pia inatapatapa kutokana na gharama kubwa ya mikopo, kwani kima cha
riba ya benki kuu kikoo juu sana, 11%, na kuifanya mikopo katika benki
za kibiashara kuwa ghali mno kwa wafanyabiashara wengi wadogowadogo,
ambao ni mhimili wa uchumi.
'Kupanda kwa gharama ya maisha'
Thamani ya shilingi iko chini kulingana na fedha
ngumu kama dola, na hivyo kuyafanya maagizo kuwa ghali zaidi, mfano
petrol au magari ambayo huagizwa kutoka nje.
Matokeo yake ni nauli kuwa juu na bei za vitu
kupanda, japo serikali inasema inadhiiti vyema mfumko wa bei ambao uko
kasoro ya 6%.
Ingawaje serikali ya Uganda, inatazamia mafuta
kuanza kuuzwa mwaka huu wa fedha, huenda ikaamua kugharamia matumizi
yake muhimu si kwa kupandisha zaidi kodi, bali kwa kupata mikopo katika
masoko ya fedha ndani na nje ya Uganda.
Kwa mfano, mikopo inachangia kasoro ya 30% ya
zao ghafi la ndani Uganda - ni kiwango cha chini, kulinganisha na Kenya
50% na Tanzania 40% hivi.
Ingawaje, mfuko wa fedha wa kimataifa, IMF na Benki ya Dunia na wadeni wengine wataiwasa Uganda isiandame mkondo huo wa madeni.