Thursday, 10 April 2014

BUNGENI KUWAKA MOTO LEO



Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta
Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na vikao vyake leo, huku wajumbe wake wakitarajiwa kuanza kusikiliza ripoti ya mambo yaliyojadiliwa katika kamati 12 zilizokuwa zikichambua sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba kabla ya kuanza kuzijadili
.

Wakati hayo yakisubiriwa, mbali na suala la muda kuonekana kuwa ni changamoto katika kujadili yaliyomo kwenye sura hizo mbili za rasimu ya katiba yenye ibara 172, mjadala mkali unatarajiwa kuligubika Bunge hilo.

Sura hizo zinazohusu muundo wa serikali, ambao umekuwa ukivuta hisia za watu ndani na nje ya Bunge hilo.

Wakizungumza na NIPASHE mjini Dodoma kwa nyakati tofautijana kuhusu namna walivyojipanga na iwapo muda unaweza kuwa changamoto, walisema huenda uwasilishaji wa ripoti za kamati usikamilike wiki hii.

Akielezea hofu ya muda, mjumbe kutoka kundi la wajumbe 201, Evod Mmanda, alisema  Bunge linahitaji saa 12 kusikiliza ripoti za kamati zote.

Lakini pia litatumia saa sita kusikiliza maoni kinzani kutoka kamati zote 12, hivyo jumla zinakuwa saa 18 kukamiliza kazi hiyo.

“Kuna saa nzima ya kuwasilisha ripoti kwa kila kamati. Pia dakika 30 kusikiliza maoni kinzani ya kila kamati. Hivyo, ni saa. Bunge linafanya kazi saa nane kwa siku.

Sijui kama  kazi itamalizika wiki hii,” alisema Mmanda. Alisema pamoja na kuwasilisha ripoti na maoni kinzani, kuna kutoa ufafanuzi, wakati mwingine utahitajika mwongozo wa mwenyekiti na kutoa taarifa, ambavyo vitakayochangia kupoteza wakati.

Mmanda alisema mashaka ya muda yanaonekana zaidi kwenye hoja ya muundo wa serikali na suala la Muungano, kwani eneo hilo limekuwa kama mada kuu kwenye  mjadala wa rasimu ya katiba.

“Kuna wasiwasi wengi wakavutiwa na kutumia muda mwingi zaidi kujadili masuala hayo,” alisema Mmanda.

Lakini kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, John Joel, alisema hakuna haja ya hofu, kwani wajumbe wanaweza kutumia muda huo na ukawatosha kwa kuwa kuna utaratibu wa kutengua kanuni na kuongeza muda wa kazi.

Joel aliwataka wajumbe kutokuwa na mashaka, kwani mwenyekiti ana utaratibu wa kutunza na kufidia wakati na kutoa mfano wa matumizi ya dakika 30 za mwenyekiti.
Mjadala wa mambo yaliyojadiliwa kwenye kamati, utaanza baada ya ripoti zote 12 kuwasilishwa bungeni na kutolewa ufafanuzi.

Kwa mujibu wa Mmanda, huenda kazi ya kujadili kazi za kamati ikaanza Jumatatu wiki ijayo.

MJADALA MUUNGANO KUTAWALA
Katika hatua nyingine;  kamati sita kati ya 12 za Bunge Maalum la Katiba zimekabidhi ripoti zake za taarifa za mijadala ilizofanya  kuhusiana na sura ya kwanza na sita ya Rasimu ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni huku suala la muundo wa Muungano likiibua mvutano mkubwa.

Kamati hizo ziliwasilisha ripoti zao kwa mujibu wa kanuni ya 32 (1) ambayo inazitaka baada ya kukamilisha midala kukabidhi taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge. Ripoti hizo zilipokelewa bungeni mjini Dodoma jana na Naibu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan.

Kamati zilizokabidhi ripoti zao jana ni namba tano inayoongozwa na Hamad Rashid Mohamed,  namba tisa inayoongozwa na Kidawa Hamisi Salehe, namba 2 inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha, namba 11 inayoongozwa na Anne Kilango, namba 12 inayoongozwa na Paul Kimiti na namba 10 inayoongozwa na Anna Abdallah.

Kukabidhiwa kwa ripoti hizo sasa  kutaliwezesha Bunge la Katiba kuanzia leo kupokea na kujadili taarifa zilizomo  kisha wajumbe wa bunge hilo kupiga kura kukubali mapendekezo yaliyopo au la.

Akiwasilisha ripoti ya kamati yake, Hamad, alisema wamefanya hivyo baada ya kufanya mjadala wa kina kuhusiana na sura hizo na kwamba wakati wa upigaji kura theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande zote mbili wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar walipitisha kwa theluthi mbili ya kura.

Kwa upande wake, Kidawa, alisema majadiliano yalienda vizuri kwenye kamati yake ambapo wajumbe walibishana kwa hoja na hatimaye kupiga kura ambapo teluthi mbili imepatikana kwa sura zote na ibara zake.

Naye Nahodha alisema mjadala kwenye kamati yake wakati mwingine ulikuwa mkali na kwamba wameshindwa kukubaliana katika masuala kadhaa.

Alisema katika sura ya kwanza inayohusu jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upande wa Zanzibar haikupatikana theluthi mbili ya kura lakini upande wa Tanzania Bara ilipatikana theluthi mbili.

Alisema kwa sura ya sita (4) kinachohusu utii wa katiba upande wa Tanzania Bara haikupatikana theluthi mbili lakini kwa Zanzibar ilipatikana theluthi mbili. Aidha, alisema Ibara ya 60 kuhusu muundo, upande wa Tanzania Bara haikupatikana theluthi mbili lakini kwa upande wa Zanzibar ilipatikana na Ibara ya 61 kwa upande wa Zanzibar haikupatikana theluthi mbili lakini kwa upande wa Tanzania ilipatikana, hivyo kwa masuala yaliyoshindikana wanaliachia Bunge zima kuamua.

Akitoa maelezo ya kamati yake, Kilango, alisema kulikuwa na mvutano mkali kuhusu muundo wa Muungano baadi wakitaka uwe wa shirikisho na wengine wakitaka wa sasa uendelee.

Alisema kwenye sura ya kwanza upande wa Zanzibar haikupatikana theluthi mbili ya kura lakini kwa upande wa TTanzania Bara ilipatikana.

Kuhusu sura ya sita inayozungumzia muundo wa Muungano, Kilango, alisema upande wa Zanzibar haikupatikana theluthi mbili na kwamba kamati yake inalichaia Bunge zima kuamua jua ya masuala hayo.

Naye Kimiti, alisema kwenye kamati yake kulikuwa na malumbano makali juu ya hati ya muungano, lakini baada ya kuitwa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa, kutoa ufafanua hali ilitulia na wajumbe walipitisha sura zote mbili kwa pande zote Tanzania Bara na Zanzibara kupata theluthi mbili ya kura.

Anna Abdallah  alisema, kwenye kamati yake,  misimamo ya makundi ilionekana bayana wakati wa mjadala na kusababisha mvutano mkubwa na kwamba  kwenye muundo wa muungano upande wa Zanzibar haikupatikana theluthi mbili ya kura.

Hata hivyo, alisema kamati yake imeongeza baadhi ya mambo kuhusiana na mipaka ya nchi kwa kuongeza mito, maziwa na anga.

Akizungumza   baada ya kupokea ripoti hizo, Samia, alizipongeza kamati hizo kwa kukamilisha kazi kwa wakati na kwamba zitawasilishwa kwenye Bunge zima kwa ajili ya mjadala.

Alisema kwa kamati nyingine sita ambazo hazijawasilisha ripoti zao zitafanya hivyo leo kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge hilo.

Kuhusu ratiba ya masuala yatakayofanyika leo, Samia, alisema Kamti ya Uongozi wa Bunge Maalum la Katiba ilitarajiwa kukutana jana usiku ilikupanga mambo mablimbali ikiwamo suala hilo.

Wakati kamati zinaanza kuwasilisha taarifa bungeni leo, kuna taarifa kwamba huenda kabla ya uwasilishaji, baadhi ya wajumbe hususani wa upinzani wakataka miongozo kuhusiana na masuala kadhaa yakiwamo malalamiko ya kupatiwa hati ya Muungano na mengine kuhusu mambo yaliyotokea katika kamati


No comments:

Post a Comment