Saturday, 5 April 2014

Ibara muhimu sura ya kwanza na sita zakataliwa na wajumbe


Mwenyekiti wa Kamati Namba sita, Steven Wassira

Baadhi ya ibara muhimu za sura ya kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba zimekataliwa na wajumbe wa kamati mbalimbali za Bunge Maalum la Katiba baada ya kukosa theluthi mbili kutoka kila upande wa Muungano Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa wenyeviti wa kamati hizo imeshindikana kutoa uamuzi kutokana na kanuni kuelekeza idadi ya wajumbe wanaopaswa kufanya maamuzi kufikia theluthi mbili kutoka kila upande.

Sura ambayo inaleta utata katika kamati zote za bunge ni sura 1(1) ambayo inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye Mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa mwenyekiti wa Kamati Namba sita, Steven Wassira, alisema wajumbe hao wameamua kuwa hoja ya kuwapo kwa serikali tatu si kutatua kero za Muungano bali changamoto hizo zirekebishwe katika serikali mbili. Alisema wajumbe waligawanyika katika eneo hilo ambapo wapo waliounga mkono shirikisho na wengine walipinga kwani katika muda wa miaka 50 kulikuwa na changamoto zilizohitaji mfumo mpya.

“Kundi la pili pamoja na kukubali kuwa kuna kero lakini walikubaliana vilevile na walitoa hoja kuwa kulikuwa na juhudi kubwa katika kuondoa kero kiasi kwamba hawadhani kwamba kubadili mfumo kunaweza kuondoa kero badala yake waliamini kwamba hata ukileta mfumo wa namna gani hauwezi kukosa changamoto.

“Walisema kero zipo na zinashughulikiwa lakini zipo kero za kikatiba ambazo kwa kweli zisingeweza kushughulikiwa bila ya mjadala wa katiba ambao tunaendelea nao,” alisema.

Alisema katika hoja zinazotolewa juu ya kero zinasema kwamba Tanzania Bara imevaa koti la Muungano kwa hiyo inaweza kuwa inafaidi zaidi kutokana na masuala ya Muungano.

“Kutokana na hali hiyo tulijadili masuala hayo ya kikatiba juu ya maeneo, mambo ya Muungano ambayo ni 11 ingawa yanaendelea kuongezeka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki…lakini kwa sababu sasa tunatazama suala la Muungano ni vizuri utakapofika wakati wake tutazame ni mambo gani ambayo tukiyaondoa katika Muungano na yakashughulikiwa na Zanzibar yanaweza yakakidhi mahitaji hayo,” alisema.

Alieleza kuwa ili kufanya maamuzi ya kifungu hicho walifikia muafaka wa kupiga kura katika eneo hilo na Tanzania Bara ilipata kura 21 sawa na asilimia 66 ambayo ni theluthi mbili na Zanzibar walipata kura 12 ikawa na upungufu wa kura moja ili iweze kupata theluthi mbili.

“Kwa hiyo hapo ndipo tulipofika…na tukakubaliana kuwa hapo tumemaliza mjadala huo na tukaendelea na vifungu vinavyofuata,” alisema.
Kuhusu kifungu cha pili kinachohusu masuala ya Jamhuri, alisema wajumbe waliona kwamba kilivyoandikwa hakikutosheleza hivyo waliamua kuwaweka wataalamu wa kisheria.

“Bahati nzuri katika kamati yangu tumebahatika kuwa wataalamu wa Sheria ambao ni Jaji Frederick Werema na Ismail Jusa Ladhu na wengine ili kulipitia suala hilo,” alisema
Alisema walichofanya katika kifungu hicho ni kuelezea na kuifafanua mipaka inayozungumzwa katika ibara hiyo ya pili.

Katika ibara hiyo inasema, eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari.

Wassira alisema ibara hiyo ilikubaliwa na pande zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema katika ibara ya tatu ambayo ilikuwa inahusu alama za taifa na sikukuu za taifa, kuna baadhi ya wajumbe walisema kuwa sikukuu nyingine si za kimuungano kwa hiyo zinatakiwa kuondolewa kwenye katiba.

“Kwa mfano Sikukuu ya Uhuru wa Tanganyika na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba tungeziondoa…lakini tulikubaliana bila Uhuru wa Tanganyika na bila Mapinduzi ya Zanzibar tusingekuwapo na Jamhuri ya Muungano…kwa sababu Jamhuri ya Muungano msingi wake ni Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar…kwa hiyo kuweka sikukuu hizi kwenye katiba ni jambo la msingi,” alisema.

Alisema walichukua muda kidogo kwa ajili ya kujadili ibara ya tunu za taifa ambapo pande zote mbili zilikuwabaliana na kipengele hicho.
Aliongeza kuwa pia walijadili ibara 6 (2) kuhusu mamlaka ya wananchi ambapo walikubaliana kuwa wananchi ndiyo wenye mamlaka ya nchi.

“Katika ibara ya saba ulizuka mjadala kidogo kuna kitu kinaitwa watu na serikali…serikali inahusianaje na watu na watu wanatarajia nini kutoka kwa serikali…hapa tulipata mjadala kidogo,” alisema
Alisema mjadala huo ulizuka kwa sababu wawakilishi wa wakulima na wafugaji waliopo kwenye kamati hiyo walipaza sauti zao kwa madai kuwa kifungu hicho hakitoshi na hakikuelekeza kwa uwazi juu ya matumizi ya ardhi kama rasilimali ya msingi kwa wananchi.

Alisema wajumbe hao walitaka bunge maalum liweke sura mahususi juu ya ardhi na rasilimali zake na pia lielekeze katiba hiyo itavyolinda rasilimali za taifa ikiwamo ardhi, madini, gesi pamoja na maliasili nyingine.

Kwa upande wa sura ya sita, alisema walijadili na kuchukua siku nzima kwani tofauti zilikuwa zile zile kama ilivyokuwa kwenye shirikisho na muungano.
Wassira alisema hoja iliyotolewa na wajumbe hao katika sura hiyo ni kwamba Tanganyika kuvaa koti na Muungano.

“Hapa tulisema kama ni koti tu basi tutalivua kwa mujibu wa katiba ili zile kero zinazoshughulikiwa na Zanzibar zishughulikiwe na Zanzibar…maana suala linalozungumzwa hapa na mambo ya mahusiano,” alisema.

No comments:

Post a Comment