Saturday, 5 April 2014

Jaji Ramadhani: Wajumbe acheni kulumbana


Makamu mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Augustino Ramadhani akiongea jijini Dsm katika mjadala kuhusiana na umuhimu wa Tanzania kuwa na katiba mpya ya kipekee.

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji mstaafu Augustino Ramadhani, amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuacha kulumbana badala yake wajadili vipengele vya rasimu hiyo.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es salaam wakati wa mjadala kuhusiana na umuhimu wa Tanzania kuwa na katiba mpya ya kipekee, ulioandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya OSIEA.

Jaji Ramadhani alisema tume ilifanya kazi ya kuwasikiliza wananchi na kuandika rasimu ambayo kwa sasa ipo mbele ya wajumbe hao na kuwashauri waijadili kwa makini ili kutengeneza mustakabali wa Tanzania kwa kuzingatia hoja na kila upande wa Muungano.

“Sisi tume tumefanya kwa kadiri ya uwezo wetu na tumepata rasimu ya pili sasa ni jukumu la wajumbe wa bunge la katiba kujadili na kuboresha vipengele vilivyomo kwenye rasimu hiyo na kuachana na malumbano,” alisema na kuongeza:
‘Kila mmoja akitaka kipengele chake kiwemo kwenye rasimu ni jambo lisilowezekana kinachotakiwa ni wajumbe kujadili na kupendekeza mambo yenye maslahi kwa taifa kwa sasa na baadaye,” alisema.

Alisema vipengele vinavyoshindaniwa vinafahamika, na wajumbe wanaweza kutumia busara kuvijadili na kuvitolea maamuzi kwa manufaa ya nchi ambayo inasubiri kwa hamu katiba mpya.

Kwa upande wake Kamishna wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar –ZEC, Dk Nassor Seif Amour aliwataka wajumbe hao kuzingatia matakwa ya wananchi badala ya kujadili maoni yao binafsi ama ya vyama wanavyoviwakilisha.

No comments:

Post a Comment