Friday, 4 April 2014

Mtambo wa kudhibiti simu uliozinduliwa na JK wakabiliwa na changamoto


Meneja wa Mawasiliano wa TCRA,Innocent Mungy.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema mtambo uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kudhibiti udanganyifu katika mitandao ya simu za kimataifa, unakabiliwa na changamoto ikiwamo kutokuwa na uwezo wa kubaini uhalifu wa simu unaofanywa ndani ya nchi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Prof. John Nkoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya mtambo huo katika kudhibiti matumizi mabaya ya simu.

Akifafanua, Mungy, alisema mtambo huo unaojulikana kama Telecommunication Traffic Monitering System (TTMS), ulianza kutumika nchini Oktoba mwaka jana, huku ukiwa na uwezo wa kubaini mitandao ya mawasiliano ya simu yanayotoka nje pekee na kushindwa kwa yale ya ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa Mungy, mtambo huo ambao unafungwa na mfumo wa kudhibiti udanganyifu (Anti-fraud management system), una uwezo wa kutambua mawasiliano ya udanganyifu katika mitandao na namba za ulaghai za nchi zinazotumika kuruhusu kupitisha mawasiliano ya kimatifa nchini kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kudhibiti mawasiliano ya simu.

Kutokana na hilo alisema, TCRA kwa ushirikiano na watoa huduma za simu na vyombo vya usalama inafanya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini uwapo wa udanganyifu huo ambao pamoja na masuala ya kiusalama, lakini pia unaikosesha mapato serikali.

“Kumekuwa na kampuni na watu binafsi wanaowezesha simu zinazopigwa kutoka nje kufika nchini bila kupitia kwenye njia rasmi na hivyo kuikosesha serikali na kampuni za simu mapato halisi.

Watu hawa hutumia ‘internet’ kuruhusu simu zinazopigwa kutoka nje ya nchi na kuzifanya zionekane kama zimetoka hapa nchini kwa kutumia kifaa kinachojulikana kwa jina la Sim Box,” alisema.

No comments:

Post a Comment